London: Kura ya maoni ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, imefungua pazia na kutoa nafasi ya kuwa na mfumo mpya wa uongozi wa nchi hiyo. Waziri Mkuu David Cameron kaachia ngazi katika nafasi hiyo baada ya kushindwa kushawishi raia wa nchi kubaki katika Umoja wa Ulaya.
Cameron ataendelea kuwa madarakani mpaka oktoba wakati uongozi mpya ukijiandaa kuchukua nafasi yake.
Cameron ameonekana kuwa mwenye majonzi kiasi cha kuwafanya waandishi wa habari waliokuwa wakimsikiliza kukaa kimya na kwa utulivu sana, hasa alipoongea kwamba anaipenda sana nchi yake na kwamba angependa kuingoza hasa katika wakati huu wa mpito.
Baadhi ya wananchi waliongea na Tanzania Nzima Media wanasema hili ni fundisho kwa Umoja wao Afrika AU, “Kama nchi zilizopo katika umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na viongozi ni muhimu kuheshimu demokrasia,” Peter Mawazo mkazi wa Dar es Salaam, “na uamuzi wa raia kuhusu mambo mbalimbali uheshimiwe pia”.
“Kwa mfano Tanzania, kura ya maoni ya rasimu ya katiba mpya watu wanaona imejaa ubabaishaji,” Asha Hafidhi, kutoka Mbagala, “ni vyema serikali kuheshimu sauti za raia wake” anasema Asha.
Katika nchi za Maziwa Makuu, kwa mfano, sauti za wananchi zimekuwa zikizimwa katika sanduku la kura. Wachambuzi wameenda mbali na kusema kazi ya raia imekuwa ni kupiga kura, lakini uamuzi wa nani awaongoze ni uamuzi wa Serikali zilizopo madarakani. baadhi ya viongozi kuendelea kutumia ujanja kubaki madarakani na kupuuza sauti za watu hali inayoongeza migogoro, wakimbizi, na vita.
“Kwa sasa kumeibuka hali ya raia kuminywa haki ya kujieleza miongoni mwa mataifa ya Afrika”, Magulu Othmani mfanyabiashara Dar es Salaam, na anaendelea, “vyama vya siasa hasa vya upinzani vinazuiwa kufanya mikutano na wananchi kupigwa pale wanapofanya maandamano ili kufikisha ujumbe wao”.
Vyama vya upinzania vimenyoshewa kidole kwa kutumia kile wanachokiita “nguvu ya umaa” kuvuruga mifumo sahihi ya demokrasia. Mbaya zaidi viongozi wengi hawako tayari kujihulu wanaposhindwa kutumiza wajibu wao.