Wakati mjadala ukiendelea nchini Tanzania kuhusu matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge, leo utafiti mpya umechochea mjadala wa suala hilo. Utafiti huo umeonesha kuwa asilimia 46 ya wananchi waliohojiwa wanataka kuwafuatilia wabunge wao moja kwa moja.
Taasisi ya Twaweza, imetoa takwimu hizo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa asilimia 79 ya Watanzania waliohojiwa hawapendi serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge. Asilimia 92 wanaona kuna umuhimu vikao hivyo virushwe moja kwa moja.
“Suala la kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Tanzania limezua mjadala mzito miongoni mwa watanzania,” amesema Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, na kuhoji, “Je, serikali iko tayari kuyapokea matakwa ya watanzania walio wengi katika jambo hili?”
Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa watu 1,815 wahojiwa kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara kati ya tarehe 29 Machi na tarehe 12 Aprili 2016. Muhtasari huo unahusisha takwimu zilizokusanywa na Sauti za Wananchi, Utafiti unaotumia simu za mkononi kwa kupata uwakilishi wa kitaifa; na mada ilikuwa “Bunge Live”.
Dondoo Muhimu:
Asilimia 46 ya wananchi wanataka kuwafuatilia wabunge wao ili kuona kama wanawawakilisha ipasavyo.
Asilimia 44 ya wananchi wanasema ni haki yao kufahamu kile kinachoendelea bungeni
- Asilimia 29 ya wananchi wanaamini zaidi matangazo ya moja kwa moja kwa sababu wanawaona na kuwasikia wabunge kwa macho na masikio yao wenyewe
- Asilimia 88 wanasema matangazo ya vikao vya Bunge yarushwe moja kwa moja bila kujali gharama. Asilimia hiyo ni kutokana na idadi ya watu waliohojiwa.
Na Josephat Mwanzi, Dar es Salaam