Dar es Salaam: ‘Mimi ndiye mbabe wa vita,” Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema hayo wakati akitangaza vita dhidi watu wanaojihusisha na ushoga, biashara ya shisha, na wavuta sigara hadharani.
“Mimi ndiye mbabe wa vita,” amesema Makonda, “ndani ya siku 7 biashara iwe imefungwa mara moja.”
Makonda kujitambulisha kuwa yeye ni ‘mbabe wa vita’ inakumbusha mbabe wa zamani wa kivita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jean-Pierre Bemba.
Bemba aliwahi kujitangaza kuwa ‘mbabe wa vita’ na anafahamika duniani kama mpiganaji wa msituni aliyetiwa hatiani hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa, ICC, kwa kosa la uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mbali na kupiga marufuku ushoga, matumizi ya shisha, na uvutaji sigara hadharani, Makonda amesema Asasi za Kiraia ambazo zinahamasisha ushoga baada ya kupokea fedha za wafadhili atazifuta mkoani mwake.
Wiki iliyopita kuna kituo kimoja cha televisheni kilirusha kipindi chenye maudhui ya ushoga lakini baadhi ya watu walilalamika katika mitandao ya kijamii kwamba kilikuwa kinatetea ushoga nchini. Wengine walisema kipindi hicho kimewasaidia kujua ukubwa wa tatizo.
Makonda ametangaza hautua hiyo ya kupambana na vitendo hivyo wakati akihutubia Tamasha la Vijana kwenye Uwanja wa Taifa. Tamasha hilo liliandaliwa na Upendo Media Group.
www.tanzanianzima.com; picha na telegrapg.co.uk